REA YAJIZATITI KUFIKISHA LENGO LA TAIFA KWENYE NISHATI SAFI YA KUPIKIA | The Dodoma Post
The Dodoma Post Tanzania

REA YAJIZATITI KUFIKISHA LENGO LA TAIFA KWENYE NISHATI SAFI YA KUPIKIA

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amesema Wakala umejizatiti kuhakikisha 80% ya Watanzania wanatumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo mwaka 2034 kama ilivyoelekezwa katika Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

Mwandishi Wetu
By Mwandishi Wetu
08 Jul 2025
REA YAJIZATITI KUFIKISHA LENGO LA TAIFA KWENYE NISHATI SAFI YA KUPIKIA

*Mkurugenzi Mkuu REA abainisha hatua zinazochukuliwa

*Amshukuru Rais Samia kwa kuwezesha

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amesema Wakala umejizatiti kuhakikisha 80% ya Watanzania wanatumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo mwaka 2034 kama ilivyoelekezwa katika Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

Amebainisha hayo Julai 07, 2025 katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) Jijini Dar es Salaam ndani ya Banda la Maonesho la Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

“REA inalo jukumu la kuhakikisha maeneo yote ya vijijini yanapata aina zote za nishati safi zinazotumika nchini ikiwemo; umeme, nishati safi ya kupikia pamoja na bidhaa za mafuta ya petroli na dizeli na hili linafanyika kupitia miradi mbalimbali ambayo baadhi imekamilika na mingine ipo katika hatua tofauti tofauti za utekelezaji,” amebainisha Mha. Saidy.

Alisema Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia umeelekeza ifikapo mwaka 2034; angalau 80% ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia na REA ni miongoni mwa taasisi zilizopewa jukumu la kuhakikisha lengo hilo linafikiwa.

Alibainisha kuwa kwa sasa takriban asilimia 96 ya wananchi maeneo ya vijijini wanatumia kuni na mkaa kupikia na kwamba jukumu lililopo ni kuhakikisha wananchi hao wanaachana na matumizi ya nishati zisizo salama na kuanza kutumia nishati safi na salama.

Alitaja hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na REA ikiwemo uhamasishaji na uelimishaji wananchi kufahamu athari za kutumia nishati isio salama pamoja na kuwafahamisha faida za kutumia nishati safi ya kupikia, kuwarahisishia wananchi upatikanaji wa bidhaa za nishati safi jirani na maeneo yao na kuwezesha teknolojia za nishati yenyewe.

“Kuna dhana imejengeka kwamba nishati safi ya kupikia ni gharama kuliko nishati zingine dhana ambayo haina ukweli kwa 100% kwani kwa sasa kuna teknolojia zilizoboreshwa ambazo zinazuia upotevu wa nishati wakati wa kupika hivyo kuwapunguzia gharama watumiaji," alifafanua Mha. Saidy

Aliongeza kuwa watu wengi hawaangalii gharama nyingine kama muda wanaotumia kusaka kuni na madhila mengine wanayokutana nayo huko porini wakati wakisaka kuni.

Alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha REA kutekeleza jukumu la kusimamia upatikanaji wa nishati safi ya kupikia hasa ikizingitiwa kuwa yeye ni kinara wa nishati safi ya kupikia.

Alibainisha baadhi ya mafanikio ambayo yamepatikana tangu kuanza kutekeleza mkakati huo wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambayo ni pamoja na kuwezesha wananchi maeneo mbalimbali vijijini kuhama kupitia ruzuku iliyotolewa ya asilimia 50 kwenye majiko ya gesi ya kilo 6 na vichomeo vyake.

“Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia ilitoa ruzuku ya 50% kwenye mitungi ya gesi ya kupikia ipatayo 452,000 ambayo imeshaanza kusambazwa kwenye mikoa yote Tanzania Bara na zoezi linaendelea; sambamba na mitungi 110,000 ambayo ilisambazwa mwaka juzi kupitia Wabunge kwenye majimbo yao,” alisema Mhandisi Saidy.

Sambamba na hilo, Mha. Saidy alibainisha kuwa REA imewezesha Jeshi la Magereza ambapo kwa sasa magereza zote 129 zimehama kutoka kwenye matumizi ya nishati zisizo salama, na hivi karibuni REA imekuja na mpango wa kuwezesha Maafisa wa Jeshi la Magereza nao kutumia nishati safi ya kupikia katika familia zao.

“Kama mtakumbuka Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alielekeza taasisi zinazohudumia zaidi ya watu 100 zianze kutumia nishati safi ya kupikia na hili tunatekeleza na tunatarajia kuzifikia zaidi ya taasisi 400 katika mwaka huu wa fedha. Tulianza na Jeshi la Magereza, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na takriban shule 53,” alibainisha Mha. Saidy.

Mhandisi Saidy vilevile alibainisha mradi wa mikopo nafuu wa kuwezesha ujenzi na uendeshaji wa vituo vya mafuta ya petroli na dizeli ulioanzishwa na REA ambao umelenga kuwasogezea wananchi wa vijijini huduma kwa gharama nafuu na ubora unaokubalika.

MKURUGENZI TASAC AWATAKA WANANCHI KUSOMA MASOMO YANAYOHUSU SEKTA YA BAHARI.

MKURUGENZI TASAC AWATAKA WANANCHI KUSOMA MASOMO YANAYOHUSU SEKTA YA BAHARI.

SHERIA ZILIZOTAFSIRIWA KWA LUGHA YA KISWAHILI KUTOKA MWEZI AGOSTI.

SHERIA ZILIZOTAFSIRIWA KWA LUGHA YA KISWAHILI KUTOKA MWEZI AGOSTI.

WAZIRI KIKWETE AIPONGEZA OFISI YA MSAJILI WA HAZINA.

WAZIRI KIKWETE AIPONGEZA OFISI YA MSAJILI WA HAZINA.

NISHATI SAFI YA KUPIKIA NI AJENDA YA DUNIA, WIZARA INAITEKELEZA KWA VITENDO - DKT. KAZUNGU.

NISHATI SAFI YA KUPIKIA NI AJENDA YA DUNIA, WIZARA INAITEKELEZA KWA VITENDO - DKT. KAZUNGU.

UDOM KUJA NA TEKNOLOJIA MPYA YA KUUZA VIMIMINIKA.

UDOM KUJA NA TEKNOLOJIA MPYA YA KUUZA VIMIMINIKA.